15/03/2022
Mbeya the Green City - Fursa za ki Uchumi
Mkoa wa Mbeya unatajwa kwa jina la utani la ‘The Green City’ yaani mji wa kijani, kutokana na kubarikiwa mvua nyingi inayoifanya mimea mingi kubakia katika hali ya kijani kibichi karibu kipindi chote cha mwaka.
Kwa hali ilivyo, ni miongoni mwa mikoa michache ambayo ni ngumu kukumbwa na baa la njaa, kwani una mazao ya aina nyingi yanayolimwa na kuvunwa kwa nyakati tofauti na kutoa fursa za kuwapo kwa kipato wakati wote.
Mbeya ina fursa nyingi ambazo mpaka sasa hazitumiki na zingine hazijaibuliwa. Mojawapo ya fursa hizi ni zile zinazopatikana kwenye sekta za kilimo na ufugaji.
Fursa za kiuchumi
Wengi wanaamini kwamba ukitaka kuwa mmoja wa matajiri Mbeya, unaweza kufanikiwa k**a utaamua kwa akili, nguvu na moyo wote kufanya kile kilichopangwa mbele yako.
Mbeya ni maarufu kwa kilimo cha mazao ya chakula ambayo yanahitaji fursa za kujengwa viwanda vya kuyasindika.
Miongoni mwa mazao hayo ni mpunga, mahindi ndizi, maharage, njugu, ngano, kunde, njegere, machungwa, matikiti maji, na mazao ya viungo vya aina mbalimbali hususan nyanya, vitunguu, pilipili, tangawizi, bizari, iriki na hata bamia.
Mkoa wa Mbeya una fursa kubwa ya kilimo cha umwagiliaji katika mabonde ya Usangu na Kyela, kwa mazao ya biashara pamoja na chai, kahawa, cocoa, chikichi, tumbaku na upandaji wa miti ya mbao, huku fursa za viwanda vya kusindika mazao hayo zikihitajika zaidi.
Kwa hali hiyo ipo fursa kubwa ya kuanzishwa kwa viwanda vya pembejeo, mbolea, na dawa za mimea kwa mifugo.
Mkoa una miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali na pia unatekeleza mradi wa kujenga na kukarabati maghala ya mahindi na mpunga katika halmashauri za Mbeya, Mbarali na Kyela.
Fursa za ufugaji
Mkoa hauko nyuma katika masuala ya ufugaji kwani una mifugo mingi, ikiwemk ng’ombe, mbuzi, na pia una mabwawa ya kufuga samaki.
Hata hivyo licha ya kuwapo mito mingi inayoingia kwenye Ziwa Nyasa na mabwawa ya asili yakiwa na samaki mpaka sasa mkoa hauna kiwanda cha nyama wala samaki.
Masoko ya ndani
Pamoja na Mkoa wa Mbeya kuwa na mazao ya aina nyingi, lakini mpaka sasa una masoko 49 na magulio 35 ambayo nayo yanatumiwa na wachache . Ipo fursa kubwa ya kuongeza masoko yanayoweza kutumika k**a fursa za kuuza na kununua bidhaa mbalimbali.
Usafirishaji
Mkoa wa Mbeya umejaliwa kwa barabara nyingi za lami zinazounganisha karibu wilaya zake zote.
Ubora wa barabara hata za wilayani unasababisha kuwapo usafiri wa kutosha wa mabasi kuelekea wilaya mbalimbali ya mkoa k**a wilaya za Kyela, Rungwe na Mbarali.
Mkoa pia umepitiwa na reli ya Tazara ambayo inatoa fursa ya kusafirisha mizigo kutoka na kwenda mikoa ya Pwani na nchi za Kusini mwa Afrika kupitia Zambia.
Hali kadhalika mkoa unacho Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Songwe (Sia) kilichopo kilometa 20 kutoka katikati ya Jiji la Mbeya.
Kiwanja hicho kina uwezo wa kupokea ndege kubwa, jambo ambalo sasa linatoa fursa kwa wafanyabiashara, wakulima na wawekezaji kufika hapa bila wasiwasi.