20/08/2023
Baba alinisisitizia kuchukua likizo kazini nirudi nyumbani nikamuone. Na alitaka nikae huko mwezi mmoja. Nilikua na mambo mengi sana kazini na nikamwambia sitaweza kupumzika kazi mwezi mzima. Lakini aliniambia mwezi mmoja wa kung'ang'ania kazi naweza kuujutia maisha yangu yote.
Kwa namna alivyokua anaongea niliogopa. Baba yangu hakua mtu wa kudekadeka. Mara nyingi alijifanya 'mgumu' hata alipokua anaumia sana. Nilipomsikia anaongea vile nilijua nahitajika kwenda kumuona. Nikachukua likizo nikaenda.
Nilifika nyumbani nikamkuta yupo hoi kitandani. Kweli alikua anaumwa, alikua kaisha, alikua kakonda, afya imedhoofu na alikua hawezi hata kunyanyuka. Alikua mpole, anaongea taratibu na mnyonge sana. Kwa mtu aliyekua anamfahamu angemuonea huruma na hata kutoa machozi. Nilimuangalia kwa huruma lakini alilazimisha tabasamu, hakutaka kuonekana mnyonge.
Aliniambia "Wewe ndiye mtoto wangu wa kwanza. Una wadogo zako sita. Wa k**e wawili na wa kiume wanne. Kuna kitu nataka nikufundishe kabla sijafa ili uje kuwa baba bora kwa wanao na si kuwa k**a mimi"
Nilimuitikia nikidhani kuwa kuna kitu ataniambia, lakini mpaka likizo inaisha hakuniambia kitu chochote. Nilishangaa na kumuuliza mbona kaniahidi kuniambia kitu lakini hajaniambia na likizo inaisha natakiwa kurudi kazini?
Alitabasmau na kuniambia kuwa ameshaniambia. Nilifikiria sana nikijaribu kukumbuka k**a kuna kitu labda aliniambia nikakisahau lakini sikukumbuka. Nilifikiri sana sikukumbuka chochote. Nikamwambia Baba mbona sikumbuki chochote. Alitabasamu tena, huku akiongea kwa shida, kisha akaniuliza nimekaa pale siku ngapi? Niilimuambia siku 23. Akaniuliza tena wewe una shangazi wangapi? Nikamuambia wawili. Akaniuliza na Baba wadogo? nikamuambia watatu.
Akaniuliza tangu nikae hapo walishakuja mara ngapi? Nilimuambia Shangazi mmoja alikuja mara tatu, kuna mwingine kila baada ya siku mbili anakuja. Baba wadogo aliyekuja ni mmoja tu, naye alikuja mara moja kwani wote wapo mjini na familia zao.
Alitabasamu tena na kuniuliza vipi mama yako tangu uje hapa yeye kaja mara ngapi? Nilishanga ana nikadhani Baba ameanza kuchanganyikiwa.
Nikamwambia “Baba Mama mbona kila siku yuko hapa, ndiyo anakupikia, anakusafisha, anakufanyia kila kitu? Inamaana umesahau?”
Nilidhani Baba akili zimeanza kumpotea lakini alitabasamu na kuniambia “Hapana mwanangu, sijasahau kuwa Mama yako yupo hapa, ila nilimsahau kipindi namuoa. Niliendekeza ndugu na kuwajali sana. Niliwapa kila msaada waliohitaji huku Mama yako akiwa tu ndani. Sikumsikiliza, sikumheshimu, sikumjali, na nilikua nikimpiga kwa maneno tu ya ndugu zangu.
Alivumilia kwakua hakuwa na pa kwenda. Wazazi wake walishafariki na ndugu zake kila mmoja alikua na familia yake. Lakini leo yeye ndiye yupo na mimi katika hali zote na nyakati zote. Ananihudumia kwa kila kitu wakati huu ambao mimi sina pa kwenda.
Alivuta pumzi kisha akaendelea kusema "Ndugu zangu wote niliowasaidia leo wana maisha mazuri lakini wapo busy na familia zao. Hawana muda wa kuja kunisalimia. Mara chache hunipigia simu kujua naendeleaje. Lakini Mama yako ananiogesha na kunilisha kila siku. Nyie wanangu mpo huko mjini mna maisha yenu. Mnakuja kuniona mara moja moja. Siwalaumu maana najua si jukumu lenu. Nawashukuru kwa kuja kunisalimia hata kwa kupangiana zamu.
Lakini Mama yako hana cha zamu, akilala akiamka yuko na mimi. akigeuka ni mimi, akila ni mimi, akipumua ni mimi, nikijisaidia ni yeye, nikitapika ni yeye, nikidondoka ni yeye.
Zamani nilikua namuambia k**a umenichoka bado ondoka lakini leo siwezi hata kujisaidia bila yeye. Mwanangu wapende ndugu zako lakini k**a hutaki kufa kwa unyonge k**a mimi basi Mpende zaidi mke wako. Huyo ndiye Mungu alipanga mzeeke naye.
Ndugu watakuja kukusalimia tu na kukupa pole lakini wakubeba kinyesi chako ni mkeo. Mfanye abebe huku akikumbuka mema uliyomfanyia na si mateso uliyompa. Mwanangu ukimnyanyasa mwanamke lazima utateseka tu. Akitangulia kufa yeye utabaki na watoto wanaokuchukiaa kwakua ulimtesa Mama yao. Na ukitangulia wewe basi yeye ndiye atakua karibu kukuhudumia wakati wa ugonjwa. Mheshimu sana mke wako.”
Baba alimaliza kuongea, akaniambia nimuache apumzike. Siku iliyofuata niliondoka kurudi mjini lakini sikufika, nilipigiwa simu kuwa Baba yangu kafariki dunia. Nilirudi kwenye msiba, ndugu zake walikuja na kulia tena sana. Hata wale ambao hawakuwahi kuja kumsalimia hata mara moja alipokua mgonjwa walijifanya kulia sana.
Lakini baada ya siku mbili wote walirudi kwao na familia zao. Alibaki Mama tu na sisi watoto wake. Badala ya kulia nilijikuta natabasamu, nikakumbuka maneno ya Baba kuwa "Watakuja watalia lakini mwisho wa siku atabaki mkeo na wanao."